NaCoNGO YAANDAA KONGAMANO KUTATHMINI NA KUENZI MCHANGO WA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI KATIKA MAENDELEO YA TAIFA


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

BARAZA la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, limeandaa Kongamano la Kitaifa litakalofanyika jijini Dodoma kuanzia tarehe 11 Agosti 2025, katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre likiwa na kwa lengo la kutathmini na kuenzi mchango wa mashirika hayo katika maendeleo ya Taifa kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Hayo yamebainishwa leo Julai 4, 2025 na Mwenyekiti wa NaCoNGO,  Jasper Lazaro Makala akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ambapo amesema Kongamano hilo linaenda sambamba na kauli mbiu isemayo "Tunathamini Miaka Mitano ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Maendeleo ya Taifa".

Hivyo amesema ni fursa ya kuangazia mafanikio, changamoto na nafasi ya mashirika hayo katika kuunga mkono juhudi za Serikali na kwamba kongamano hilo linatarajiwa kuhudhuriwa na zaidi ya washiriki 2,000 kutoka ndani na nje ya nchi, huku Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Bw. Makala alibainisha kuwa kabla ya kongamano hilo la kitaifa, makongamano ya aina hiyo tayari yamefanyika katika ngazi ya wilaya na mikoa, na alitumia nafasi hiyo kuwashukuru viongozi kwa ushirikiano wao katika kuhakikisha mashirika hayo yanatambuliwa na kushirikishwa katika ajenda za maendeleo.

Aidha, aliwahimiza wanachama wa mashirika, wadau na wananchi watakaoshindwa kuhudhuria kongamano hilo kufuatilia matangazo ya moja kwa moja kupitia mitandao ya kijamii.

Kwa upande wake, Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Tanzania Bara, Bi. Vickness Mayao, alisema kuwa kongamano la mwaka huu lina umuhimu wa kipekee kwa kuwa linahusisha tathmini ya miaka mitano ya mchango wa mashirika haya katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

“Ni miaka mitano sasa tangu tuanze kuandaa makongamano haya, lakini mwaka huu ni wa kipekee kwa sababu tunafanya tathmini ya mchango wa mashirika haya kwa ujumla wake tangu kuanzishwa kwake,” alisema Bi. Mayao.

Naye Naomi Vicent, Meneja wa Kitengo cha Usimamizi wa Sekta Binafsi kutoka Benki ya Stanbic, alisema kuwa taasisi yao imekuwa mshirika wa karibu wa mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kuwasaidia kupitia programu za incubation zinazolenga kuendeleza taasisi changa.

“Tumeendelea kutoa usaidizi wa kitaalamu, rasilimali na ufadhili wa miradi mbalimbali, kwa lengo la kuhakikisha taasisi hizi zinakuwa imara na kuleta matokeo chanya kwa jamii,” alisema Naomi.

Kongamano hilo linatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kutathmini mafanikio, kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto na kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na sekta binafsi kwa maendeleo endelevu ya Taifa.

Post a Comment

0 Comments