SERIKALI YAPUNGUZA MIGOGORO YA ARDHI MKOANI MARA MIAKA MINNE YA RAIS SAMIA



NA MWANDISHI WETU, DODOMA

MKOA  wa Mara umepiga hatua  katika sekta ya ardhi ndani ya kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, kwa kupunguza migogoro ya ardhi kutoka 964 mwaka 2021 hadi migogoro 125 mwaka 2025 ikiwa ni mafanikio yaliyotokana na juhudi za Serikali kuboresha mfumo wa umiliki, upangaji na matumizi bora ya ardhi.

Akizungumza jijini Dodoma leo Julai 18,2025 jna waandishi wa habari wakati akielezea mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Alfred Mtambi, amesema kuwa hatua hiyo imeleta utulivu mkubwa katika jamii, hasa katika maeneo ya vijijini ambako migogoro ya ardhi ilikuwa ikichochea migogoro ya kijamii na kushusha kasi ya maendeleo.

 “Tumeweka nguvu kubwa katika kupanga, kupima na kumilikisha ardhi kwa wananchi na taasisi. Hii imeongeza uelewa, kupunguza migogoro na kuongeza mapato ya Halmashauri kupitia kodi ya ardhi,” amesema Kanali Mtambi.

Amesema, zaidi ya hati 60,969 za kimila zimetolewa kwa wananchi, sambamba na hati miliki za ardhi 6,743, hatua inayowasaidia wananchi kuwa na uthibitisho wa umiliki, na pia kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha kwa maendeleo yao binafsi na ya familia.

Katika hatua nyingine amesema mkoa umefanikiwa pia kutambua maeneo 167 ya hifadhi na mashamba ya Serikali, na kuyawekea mipaka rasmi, hatua iliyosaidia kuzuia uvamizi na matumizi holela ya maeneo ya umma.

Akizungumzia Vijiji Vyenye Mipango Bora Ya Matumizi Ya Ardhi,ameeema idadi ya vijiji vilivyopangwa na kuidhinishiwa mipango ya matumizi bora ya ardhi imeongezeka kutoka vijiji 35 mwaka 2021 hadi 218 mwaka 2025.

Amesema Mpango huu umesaidia vijiji kuwa na ramani ya matumizi ya ardhi kwa shughuli mbalimbali kama makazi, kilimo, mifugo, huduma za jamii na biashara.

Pia ameeleza kuwa hatua hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kupunguza migogoro kati ya wakulima na wafugaji, pamoja na kuimarisha huduma za kijamii kama shule, zahanati na masoko katika maeneo ya vijijini.

Licha ya hayo ameeleza kuwa Serikali imeendesha kampeni za uhamasishaji na elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kupanga na kumiliki ardhi kisheria ikiwa ni pamoja na kuimarisha Kamati za Ardhi za Vijiji  kwa mafunzo na vitendea kazi ili ziweze kusimamia ipasavyo matumizi ya ardhi katika maeneo yao.

Kupitia usimamizi bora wa ardhi na ukusanyaji wa kodi ya pango la ardhi,Mkuu huyo wa Mkoa wa Mara amesema Halmashauri zimeongeza mapato ya ndani, hali ambayo imewezesha kutekeleza miradi mingine ya maendeleo ikiwemo miundombinu ya shule, afya na barabara.

Post a Comment

0 Comments