NA MWANDISHI WETU
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imepongezwa kwa kufanya kazi nzuri ya kuwahudumia wakazi wa Mwanza na kuwahamasisha kurasimisha biashara zao.
Hayo yamebainishwa jana tarehe 2 Septemba 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Saidi Mtanda, katika uzinduzi wa Maonesho ya 20 ya Biashara ya Afrika Mashariki yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya Nyamagana, Jijini Mwanza.
Akipita katika banda la BRELA, Mhe. Mtanda alisema kuwa BRELA inafahamika kwa mapinduzi ya uboreshaji wa utoaji huduma na kuhimiza kuendelea na kazi nzuri inayofanywa na taasisi hiyo.
Katika maonesho haya, BRELA imeshinda nafasi ya tatu kati ya taasisi zote za umma zilizoshiriki na kupata cheti cha ushindi kama taasisi inayotoa huduma bora kwa wadau wake katika urasimishaji wa biashara.
Ushiriki wa BRELA katika maonesho haya unalenga kuhakikisha huduma zote za Usajili wa Majina ya biashara, Kampuni, Alama za biashara na Huduma, utoaji wa Hataza, Leseni za biashara kundi “A”, Leseni za viwanda, na Huduma za kulipia ada za mwaka pamoja na uhuishaji wa taarifa za Majina ya biashara na Kampuni zinatolewa papo kwa papo.
Banda la BRELA ni miongoni mwa mabanda ya taasisi za serikali zilizoshiriki katika maonesho haya ya Biashara ya Afrika Mashariki, kwa lengo la kusogeza huduma karibu na jamii, hasa kwa kuzingatia kuwa huduma zote zinatolewa kwa njia ya mtandao na zinapatikana papo hapo.
Pamoja na kutoa huduma za papo hapo, BRELA pia inatoa elimu kwa umma kuhusu namna ya kupata huduma zake zinazotolewa kupitia mtandao. Maonesho haya ya siku kumi na moja yalifunguliwa rasmi jana tarehe 2 Septemba 2025 na Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na yatahitimishwa rasmi tarehe 7 Septemba 2025.
Maonesho haya ya Biashara ya Afrika Mashariki yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Biashara ya Kijani, Uchumi Mzunguko, Maisha Endelevu.”
0 Comments