TLP YAAHIDI MABADILIKO IKIPATA KITI CHA URAIS UCHAGUZI MKUU 2025, kila Mtanzania kupata milo mitatu kwa siku, yazindua kampeni



NA MWANDISHI WETU

MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Yustas Mbatina Rwamugira, ameahidi kubadilisha mfumo wa kiutawala na kiuchumi nchini endapo atapata ridhaa ya Watanzania kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 huku akiisifu Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Rwamugira amebainisha hayo akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika Septemba 4, katika viwanja vya Bakhresa, Manzese, jijini Dar es Salaam ambapo amesema Serikali yake itajikita katika kusimamia utawala bora, uchumi imara na ajira kwa vijana.

Amebainisha kuwa mpango wake ni kuhakikisha hospitali zinakuwa huru dhidi ya madeni sugu yanayokwamisha utoaji wa huduma, pamoja na kuweka mikopo rafiki inayoweza kufikiwa na wananchi wa kada zote.

Vilevile, ametoa wito kwa wananchi kushiriki Uchaguzi Mkuu kwa amani na utulivu.

Katika hatua nyingine mgombea huyo, akiwa sambamba na mgombea mwenza wake Amana Suleiman Mzee, amewaeleza wananchi dhamira ya TLP kuhakikisha kila Mtanzania anapata milo mitatu kwa siku endapo watachaguliwa kuunda serikali.

Amesema azma hiyo ni sehemu ya mikakati ya chama hicho kupunguza changamoto za kiuchumi na kuinua hali ya maisha ya wananchi, huku akiwataka Watanzania kuipa kura TLP ili iweze kutekeleza sera zake kwa vitendo.

Post a Comment

0 Comments