BARA LA AFRIKA: TUNAHITAJI WANAHABARI MAHIRI KUKUZA SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UBUNIFU




Na Veronica Mrema, Pretoria 

Uandishi wa habari za sayansi kwa umakini na umahiri ni nyenzo muhimu ili kufikisha ujumbe sahihi kwa jamii, kusaidia kukuza maendeleo ya tafiti na vumbuzi mbalimbali.

Bara la Afrika bado lina uhitaji mkubwa wa waandishi wa habari ambao wamejikita na wapo na umahiri katika kuwasilisha masuala ya sayansi kwa lugha rahisi zinazoeleweka kwa jamii.

“Kazi yoyote ile tunayoifanya [katika] sayansi ina maana tu pale inapofahamika vizuri kwa watu na jamii nzima,”.

Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Afrika Kusini Profesa Blade Nzimande amesema hayo alipokuwa akifungua rasmi Mkutano wa 13 wa Waandishi wa Habari za Sayansi Duniani.

Mkutano huo WCSJ2025 unafanyika Pretoria Afrika Kusini kuanzia Disemba 1-5, 2025 ukiwa na kauli mbiu isemayo 'Uandishi wa sayansi, unaojenga uelewa na uthabiti wa sayansi na haki za kijamii'.

“Nilipoombwa kuja kufungua mkutano huu nilikubali mara moja kwa sababu ya umuhimu wa nafasi ya waandishi wa habari za sayansi katika kukuza sayansi,” amesema.

Ameongeza “Kwa hiyo waandishi wa habari ni daraja muhimu sana [lakini] hatusemi daraja lisilo na ukosoaji, hapana  bali daraja muhimu la kuielimisha jamii kuhusu sayansi.

“Kama bara, tunahitaji waandishi wa habari za sayansi wengi kwa sababu bado tunalo jukumu la kuendeleza sayansi, teknolojia na ubunifu barani Afrika.

“Na mawasiliano ni sehemu muhimu ya hilo. Kwa mfano, tunayo mkakati wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kwa Afrika [STISA 2034].

“.., ambao unalenga kukuza sayansi, utafiti na maendeleo barani Afrika jambo muhimu sana. Kwa hiyo tunathamini kazi mnayofanya, na ni muhimu sana,” amesema.

Amesema waandishi wa habari wanapaswa kusaidia Bara la Afrika kupambana na dhana potofu na ubaguzi katika namna sayansi inavyowasilishwa.

“Lazima tuwahusishe pia makundi yaliyotengwa wanawake, watu waliodhulumiwa au waliokuwa na historia ya ukandamizaji ili nao wawe sehemu ya mawasiliano ya sayansi.

“Moja ya hatari kubwa inayoweza kuua umuhimu wa sayansi ni kuifanya kuwa mradi wa viongozi au watu wachache.

“Sayansi haipaswi kuwa mradi wa tabaka la juu; lazima iwe mradi unaoeleweka na watu wote. Tunawahimiza kuhakikisha mnazingatia hilo kama waandishi wa sayansi,” amesema.

Prof. Nzimande ameongeza “Waandishi wa habari mnapaswa kukabiliana na changamoto ya taarifa za uongo [fake news].

“Hili ni mojawapo ya mambo hatari sana katika mawasiliano leo, mitandao ya kijamii ina mazuri na mabaya.

“Ni mazuri kwa kuwa kila mtu anaweza kupata taarifa  siku hizi karibu kila mtu anasema,” amesema na kuongeza  

“Mimi ni mtengeneza maudhui.” Lakini pia mitandao ya kijamii inaweza kusambaza taarifa za uongo haraka sana, jambo ambalo ni hatari.

“Katika sayansi, tunapaswa kupambana na taarifa za uongo, si tu katika jamii kwa ujumla, bali katika sayansi haswa kwa sababu inaweza kusababisha madhara makubwa.

Amesisitiza “Je, mnakumbuka wakati wa COVID jinsi taarifa za uongo zilivyosambaa?

“Leo kuna watu katika nchi kubwa wanaodai kwamba chanjo husababisha autism  jambo la uongo kabisa.

“Lakini likirudiwa na watu wenye mamlaka, linakuwa hatari zaidi. Hii ina maana kwamba lazima muwe jasiri kama waandishi.

“Mnapaswa kuwa jasiri na msiogope kuuliza maswali makubwa na muhimu,” amesema.

Teknolojia ya Akili Unde [AI] katika sekta ya habari pia si suala la kuliacha nyuma, amesisitiza,

“Tunahitaji kuingiza teknolojia mpya kama akili bandia katika kazi yenu, ili kuimarisha weledi na uwazi katika taaluma yenu.

“Tunapaswa pia kushughulikia tofauti katika namna sayansi inavyoripotiwa. Bara letu bado linatengwa katika mambo mengi.

“Mnachukua jukumu la kuhakikisha masuala ya sayansi yanawafikia Waafrika si hivyo tu.

“Bali pia kuhakikisha ubunifu, uvumbuzi na miradi ya sayansi kutoka  Afrika inatambulika ndani na nje ya bara,” amesema Prof Nzimande.

Diplomasia ya sayansi pia waandishi wa habari wanalo jukumu la kusaidia kuikuza ndani ya Bara la Afrika.

“Sayansi haina mipaka, na kwa sababu hiyo ina uwezo mkubwa wa kujenga mahusiano ya kidiplomasia baina ya nchi na mabara.

“Kama Afrika Kusini, tunaamini sana katika sayansi huria kwamba sayansi inapaswa kufikika zaidi na iwe wazi.

“Lakini lazima niseme kwamba waandishi wa habari za sayansi ni sehemu muhimu sana mjue au msijue katika kazi tunazofanya katika sekta ya sayansi.

“Bila ninyi, hatuwezi kuwafikia wale tunaopaswa kuwafikia,” amesema Prof Nzimande.

Post a Comment

0 Comments