NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)
imefanya operesheni mbalimbali zilizofanikisha ukamataji wa jumla ya kilogramu
3,799.22 za dawa za kulevya, kuteketeza ekari 18 za mashamba ya bangi pamoja na
kutaifisha mali za wahalifu wa dawa za kulevya zenye thamani ya shilingi
Bilioni tatu na milioni mia tatu na nne (3,304,000,000/=).
Hayo yamebainishwa leo Disemba 3, 2025 na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, amesema watuhumiwa 84 walikamatwa kuhusiana na dawa hizo.
“Katika kuendeleza hatua za kukabiliana na uhalifu wa dawa za kulevya, Mahakama kuu divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ilitoa maamuzi ya kutaifishwa kwa mali zenye thamani ya Tsh. Bilioni Tatu na milioni mia tatu na nne (3,304,000,000/=) za watuhumiwa Saleh Khamis Basleman na Gawar Bachi Fakir ambao wanatuhumiwa kwa makosa ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya,” amesema Kamishna Jenerali Lyimo.
Ameeleza kuwa mali hizo zinajumuisha nyumba, viwanja na
magari, kwamba maombi ya kutaifishwa kwa mali hizo yaliwasilishwa mahakamani
hapo kufuatia uchunguzi uliofanyika na ikabainika kwamba, watuhumiwa hao
wanamiliki mali ambazo zilipatikana kwa njia za uhalifu wa biashara ya dawa za
kulevya.
Amesema utaifishaji wa mali hizo umefanyika chini ya Sheria
ya Mazao ya Uhalifu Sura ya 256 ikisomwa pamoja na Sheria ya Uhujumu Uchumi na
Uhalifu wa Kupangwa Sura ya 200 na Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za
Kulevya Namba 5 ya mwaka 2015.
Amefafanua kuwa utaifishaji wa mazalia ya uhalifu umewekwa
kisheria ili kuifundisha jamii kuwa, uhalifu hauna faida na adhabu za kifungo
hazitoshelezi kutokomeza uhalifu hasa katika makosa ya kupangwa ikiwemo makosa
ya dawa za kulevya. Huu ni mkakati wa kuzuia uhalifu kuendelea na kuondoa
matamanio ya kufanya uhalifu.
Ametaja orodha ya mali zilizotaifishwa kuwa ni Apartment
Namba OA2, Ghorofa ya Kwanza, iliyopo Sea Breeze Residential Complex, kiwanja
Namba 192 Block "O", Jangwani Beach, Kinondoni, Dar es Salaam.
Mali nyingine ni Apartment 6B, kiwanja Namba 26 Block 52,
iliyopo Kariakoo, Ilala, Dar es Salaam, Nyumba iliyo kwenye kiwanja Namba 329
na 1009 Block "C", Mbezi wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam na kiwanja
Namba 69 Block 7, kata ya Mbweni JKT, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Amebainisha mali nyingine kuwa ni Nyumba Namba 14, iliyopo
kiwanja Namba 131 Block 9, mtaa wa Chui Mtoni Kijichi, NSSF House Scheme Phase
III, Temeke, Dar es Salaam, kiwanja Namba 44768, kilichopo mtaa wa Kigogo kata
ya Kisarawe II, Kigamboni Dar es Salaam na kiwanja kilichopo Shungubweni
Village, kata ya Shungubweni, wilaya ya Mkuranga, mkoa wa Pwani.
Kadhalika ametaja Kiwanja Namba 53 Block E, Boza Village, Wilaya
ya Mkuranga, mkoa wa Pwani, kiwanja kilichopo Boza village, kata ya Boza wilaya
ya Mkuranga, mkoani Pwani, kiwanja Namba 8 Block C, kilichopo mtaa wa Mwambao,
kata ya mji Mkongwe, wilaya ya Bagamoyo, mkoa wa Pwani na Apartment Namba PA1,
Ghorofa ya chini, Sea Breeze Residential Complex, kiwanja Namba 192 Block P,
iliyopo Jangwani Beach, Kinondoni Dar es Salaam.
Hakuishia hapo, nyingine ni Nyumba Namba 9, iliyopo Magomeni,
wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam, kiwanja Namba 44746, kilichopo mtaa wa Kigogo,
kata ya Kisarawe II, Kigamboni Dar es Salaam, kiwanja Namba 44748 kilichopo
mtaa wa Kigogo, kata ya Kisarawe II Kigamboni Dar es Salaam na kiwanja Namba
44789, kilichopo mtaa wa Kigogo, Kata ya Kisarawe II, Kigamboni Dar es Salaam.
Kamishna Jenerali Lyimo ametaja Magari yaliyotaifishwa kuwa
ni pamoja na, Gari namba T 539 DKQ, Nissan Civilian, Gari namba T 427 EAH,
Subaru Impreza, Gari namba T 196 EAC, Volkswagen, Gari namba T 654 DCH,
Volkswagen na Gari namba T 141 DKV, Nissan Civilian.
Mengine ni Gari namba T 944 DKY, Nissan Civilian, Gari namba
T 830 DLA, Nissan Civilian, Gari namba T 767 DLL, Nissan Civilian, Gari namba T
435 DJY, Toyota Corolla Spacio, Gari namba T 307 DLW, Nissan Civilian na, na Gari
namba T 753 DKS, Nissan Civilian.
Kadhalika, amebainisha kuwa Mamlaka hiyo imefanya operesheni
mbalimbali Jijini Dar es Salaam ambapo katika eneo la Sinza D, iliwakamata Bw.
Cuthbert Kalokola (34) na Bi. Murath Abdallah (19) wakiwa na dawa mpya za
kulevya aina ya 3,4 - Methylenedioxymethamphetamine (MDMA) vidonge 738 vyenye
uzito wa gramu 177.78 na dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Rohypnol
(flunitrazepam) vidonge 24 vyenye uzito wa gramu 10.03.
Kwamba eneo la Mbezi maramba mawili, watuhumiwa Jaribu Tindwa
(38), Ally Meshe (39), Juma Mfamo (20) Rahim Nampanda (28), Abubakari Ally
(20), Nurdin Rashid (36) na Farid Rashid (33) walikamatwa wakiwa na kilogramu
90 za dawa za kulevya aina ya skanka zikiwa zimefichwa ndani ya matanki ya
solar panel zilizokuwa zimepakiwa kwenye basi la Falcon, aina ya Scania lenye
namba za usajili T372 DFK linalofanya safari zake kati ya Tanzania na Malawi.
Vilevile, katika operesheni nyingine iliyofanyika Mkoani
Rukwa katika mpaka wa Kasesya, alikamatwa Bw. Godwin Andrew (26) mkazi wa
Mbalizi Mbeya akiwa na dawa za kulevya aina ya skanka zenye uzito wa kilogramu
244.3.
Amesema Dawa hizo zilikuwa zimefichwa ndani ya spika, mashine
za kupooza hewa, mashine za kukatia majani na vifaa vya kompyuta (CPU). Vifaa
hivyo vilikuwa vikisafirishwa katika gari aina ya Iveco Van yenye namba za
usajili wa nchi ya Afrika Kusini CN 85 FN GP mali ya kampuni ya usafirishaji ya
Makamua Logistics Limited lililokuwa likitokea nchini Afrika Kusini kuja Dar es
Salaam.
Aidha, katika operesheni zilizofanyika mikoa mingine nchini, zilikamatwa
kilogramu 2,041.45 za bangi, kilogramu 1,423.28 za mirungi na ekari 18 za
mashamba ya bangi ziliteketezwa. Magari manne na pikipiki 12 vilikamatwa katika
operesheni hizo. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inatoa
wito kwa wananchi kushiriki katika mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya
kwa kutoa taarifa za uhalifu wa dawa za kulevya.
0 Comments