Mbeto awahimiza Wafanyabishara kutopandisha bei za Vyakula kwa walaji Zbar



Na Mwandishi  Wetu, Zanzibar 

Chama Cha Mapinduzi kimewataka Wafanyabiashara kwenye Masoko kuacha kupandisha bei za bidhaa za  Vyakula  kiholela katika Mwezi  huu Mtukufufu wa Ramadhan Visiwani Zanzibar. 

CCM imewanasihi  Wafanyabiashara wenye tabia hiyo kutowakomoa walaji kwani si kitendo cha kiungwana .

Ushauri huo umetolewa na Katibu wa Kamati  Maalum  ya NEC Zanzibar ,  Idara  ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Khamis Mbeto Khamis  baada ya kutembelea Masoko kadhaa katika Kisiwa cha Unguja.

Mbeto alitoa matamshi hayo  alipotembelea  na kujionea  bei za bidhaa za Vyakula na mafuta ya kula kwenye  baadhi ya Masokona  kuwashauri watoa huduma hizo kupandisha bei kwa  walaji si jambo jema.

Alisema Wafanyabiashara  wanatakiwa kufikiria maslahi ya walaji hivyo kitendo cha kupandisha bei kiholela kwa nia ya kutaka kupata faida kubwa hakionyeshi utu na  ubinadamu.

"Nimetembelea  baadhi ya Masoko kadhaa nimekuta baadhi ya bidhaa hazijawasili toka maeneo mbalimbali  ya nchi  yetu . Kitendo cha kupandisha bei  katika Mwezi huu Mtukufu hakikubaliki" Alisema Mbeto 

Aidha Katibu Mwenezi huyo alisema pamoja na  baadhi ya bidhaa za vyakula kutoka nje ya Zanzibar kutofika sokoni katika siku za Ramadhan za  mwanzoni , kupandisha bei  ni  kuwaumiza walaji .

'Lazima Wafanyabiashara na Waagizaji wetu  watambue  kupandisha bei kubwa  bila kujali  wenzao ni ukatili. Biashara ziongozwe na utu na huruma kwa kuwafikiria  walaji  "Alieleza .

Aidha, Mbeto aliwataka watu wanaouza bidhaa kwenye Masoko,  kupunguza ukali wa maneno na  utani usiopendezesha katika jamii wakati  huu na Mwezi Mtukufu  wa Ramadhan. 

" Zanzibar inasifika   duniani kwa watu wake kuwa na  huruma ,  ukarimu na uungwana  wa watu wake .Utani na masihara  yanayopitiliza kwa baadhi ya watu kutoa maneno makali kwenye Masoko  si jambo zuri "Alisisitiza .

Hata hivyo Katibu  huyo Mwenezi  alihimiza na kuwashauri Watendaji  dhamana wa Idara za biashara  za SMZ kufuatilia kwa karibu bei za vyakula katika Masoko ya Unguja na Pemba.

Post a Comment

0 Comments