*Awasha umeme Kitongoji cha Bugofuma wilayani Misungwi
*Wananchi kufungiwa mita janja kurahisisha ununuzi wa umeme
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikisha kuwa wateja wote wanaolipia huduma ya umeme wanaunganishwa kwa wakati ili kuwawezesha kuutumia kwa shughuli za kijamii na kiuchumi.
Ametoa agizo hilo tarehe 23 Februari 2026 mara baada ya kuwasha umeme katika Kitongoji cha Bugofuma, kilichopo Kijiji cha Ngeleka wilayani Misungwi mkoani Mwanza, ambacho kimepata umeme kupitia mradi unaotekelezwa na TANESCO kwa gharama ya shilingi milioni 174, huku wateja wa awali 171 wakitarajiwa kunufaika.
“Sisi Wizara ya Nishati tumeshawaelekeza REA na TANESCO kuhakikisha kuwa katika miradi ya umeme vitongojini inayoendelea mtu akilipia leo, zisipite siku tatu hadi nne awe amewekewa umeme. Na hapa Bugofuma tumeona TANESCO wametekeleza agizo hili kwani kati ya wananchi wa awali 35 waliolipia huduma jana, tayari wananchi 22 wameunganishiwa umeme." Amesema Mhe. Salome
Ameeleza kuwa, kasi ya uunganishiaji wateja umeme ni utekelezaji pia wa Mpango Mahususi wa Taifa wa Nishati (National Energy Compact 2025–2030), unaolenga kukuza upatikanaji wa umeme kufikia asilimia 100 katika maeneo ya vijijini na mijini, pamoja na kuongeza uunganishwaji wa umeme kwa kaya hadi kufikia asilimia 75.
Mhe. Salome amemshukuru Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi thabiti na wenye kujali utu, ukiwa na azma ya kuhakikisha vitongoji vyote nchini vinapata huduma ya umeme ya uhakika na nafuu ifikapo mwaka 2030.
Katika hatua nyingine, Mhe. Salome amesema wateja wote katika kitongoji hicho watafungiwa mita janja (smart meters) zitakazowawezesha kununua umeme wakiwa popote bila ya kuhitajika kuingiza namba za token kama ilivyokuwa awali.
Katika hafla hiyo, Mhe. Salome ameziagiza TANESCO na REA kufikisha nishati ya umeme kwa taasisi zinazotoa huduma kama vile vituo vya afya, shule, vituo vya polisi na masoko, pamoja na kuendelea kuchochea matumizi ya nishati safi ya kupikia.






0 Comments