CPA MAKALLA AITAKA LONGIDO KUIMARISHA UDHIBITI WA MAPATO KUEPUKA HOJA ZA CAG



NA MWANDISHI WETU, LONGIDO

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, ameiasa Halmashauri ya Wilaya ya Longido kuhakikisha inaweka udhibiti madhubuti wa mapato ili kuepuka kujitokeza kwa hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika taarifa za fedha za Halmashauri.

CPA Makalla ametoa kauli hiyo leo Juni 26, 2026 wakati akizungumza katika Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Longido uliokuwa ukijadili utekelezaji wa hoja za CAG kuhusu taarifa za fedha za Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2025. Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri, J.K. Nyerere.

“Pamoja na kuwa mmepata hati safi, inatakiwa ithibitishwe na udhibiti wa mapato. Mnaweza mkawa na hati safi, lakini mkawa hamna udhibiti wa mapato kwa maana ya kuelekeza mapato kwenye mipango husika,” amesema CPA Makalla.

Amesema katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kila mradi unapaswa kutekelezwa kwa kuzingatia thamani ya fedha zilizotengwa na kutolewa, huku ubora wa mradi ukiendana na thamani halisi ya fedha zilizotumika.

Kutokana na hilo, Mkuu wa Mkoa ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Longido kuhakikisha inaweka mifumo bora ya udhibiti wa fedha kwa kutumia kikamilifu Mkaguzi wa Ndani na kuzingatia taratibu zote za matumizi ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Amesema hatua hiyo itasaidia kuhakikisha fedha za miradi zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuondoa changamoto zinazoweza kujitokeza katika ukaguzi wa hesabu za Halmashauri.


Post a Comment

0 Comments