LONGIDO YANG’ARA KWA HATI SAFI MIAKA MINNE MFULULIZO, RC MAKALLA ATOA PONGEZI




NA MWANDISHI WETU, LONGIDO

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Longido kwa kupata hati inayoridhisha (hati safi) katika mwaka wa fedha 2024/2025, ikiwa ni mwaka wa nne mfululizo kwa Halmashauri hiyo kupata mafanikio hayo.

CPA Makalla ametoa pongezi hizo leo Juni 26, 2026 wakati akizungumza katika Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Longido uliokuwa ukijadili utekelezaji wa hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu taarifa za fedha za Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2025. Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri, J.K. Nyerere.

“Niwapongeze Halmashauri ya Wilaya ya Longido kwa kupata hati safi, lakini pia nipongeze Halmashauri zote saba za Mkoa wa Arusha kwa kupata hati safi. Nijipongeze kama Mkuu wa Mkoa nimeanza vizuri kwa Halmashauri zote kuwa na hati safi. Hivyo naomba tuendeleze hili,” amesema CPA Makalla.

Amesema kupata hati safi kunatoa matumaini na imani kwa wananchi kuwa fedha wanazozitoa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo zinasimamiwa vizuri na zipo salama.

Mkuu huyo wa Mkoa ameeleza kuwa aliwahi kufanya kikao na madiwani na kukubaliana kuhakikisha Halmashauri zote zinaendelea kupata hati safi. Ameongeza kuwa ingekuwa ni jambo la kusikitisha kwake endapo Halmashauri zingepata hati chafu, kwani ingekuwa ni ishara ya kushindwa kutumia taaluma yake katika kutoa ushauri wa kuzuia changamoto hizo.

Hata hivyo, CPA Makalla amesisitiza kuwa pamoja na kupata hati safi, Halmashauri zinapaswa kuimarisha udhibiti wa mapato ili kuepuka kujitokeza kwa hoja za ukaguzi. Amesema Halmashauri inaweza kupata hati safi lakini bado ikawa na hoja endapo kutakuwa na udhibiti hafifu wa mapato.


Post a Comment

0 Comments