LONGIDO YAREJESHA ZAIDI YA SHILINGI MILIONI 542 ZA MIKOPO YA ASILIMIA 10 YA HALMASHAURI

NA MWANDISHI WETU, LONGIDO

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido mkoani Arusha, Mhe. Thomas Ngobei, ameipongeza Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Longido pamoja na Idara ya Maendeleo ya Jamii kwa kufanikisha urejeshwaji wa shilingi milioni 542,036,700 hadi kufikia Mei 2026, kati ya deni la shilingi milioni 648,846,700 la mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri inayotolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Mhe. Ngobei ametoa pongezi hizo leo Juni 26, 2026 wakati akizungumza katika Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Longido uliokuwa ukijadili utekelezaji wa hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu taarifa za fedha za Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2025. Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri, J.K. Nyerere.

“Niwapongeze Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Idara ya Maendeleo ya Jamii kwa kufanikisha kurejeshwa kwa kiasi hiki. Ninaamini kiasi cha shilingi milioni 106,783,000 kilichobaki si kikubwa na kitarejeshwa na kukamilishwa kwa wakati,” amesema Mhe. Ngobei.

Mwenyekiti huyo ametumia fursa hiyo kuwataka Waheshimiwa Madiwani kuwa karibu na wananchi katika maeneo yao na kuwahimiza kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kuwawezesha wananchi wengine pia kunufaika na mikopo hiyo.

Aidha, Mhe. Ngobei amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii ngazi ya Kata kuimarisha ufuatiliaji na usimamizi wa vikundi vinavyonufaika na mikopo hiyo kwa kuhakikisha daftari za mikopo, ratiba za marejesho pamoja na kumbukumbu za wanufaika zinatunzwa kwa usahihi, zinafanyiwa maboresho mara kwa mara na kupitiwa kwa utaratibu.


Post a Comment

0 Comments