TFS YASHIRIKI MAONESHO YA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA DODOMA




Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) unashiriki Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea kitaifa katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma kuanzia Juni 16 hadi 23, 2026, kwa lengo la kutoa elimu na kuonesha huduma mbalimbali zinazotekelezwa katika sekta ya misitu.

Kupitia maonesho hayo, wananchi wanapata fursa ya kujifunza kuhusu shughuli za uhifadhi na usimamizi endelevu wa misitu, uzalishaji wa mazao ya misitu, utalii wa misitu, pamoja na fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana katika maeneo ya misitu iliyohifadhiwa nchini.

Aidha, TFS inatoa huduma na elimu kuhusu udungishaji wa nyuki (Bee Venom Therapy/Apitherapy), tiba asilia inayotumia sumu ya nyuki, ambapo wananchi wanapata ufafanuzi kutoka kwa wataalamu wa wakala huo kuhusu matumizi na manufaa ya huduma hiyo, sambamba na bidhaa zitokanazo na mdudu nyuki.

Mhifadhi Mkuu wa TFS, Kassim Ally, amewahimiza wananchi kutembelea banda la wakala huo katika maonesho hayo ili kupata elimu, ushauri wa kitaalamu na taarifa kuhusu fursa za utalii wa misitu na uwekezaji, pamoja na kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Serikali kupitia TFS katika kuhifadhi, kusimamia na kuendeleza rasilimali misitu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Post a Comment

0 Comments