UMEME UPO WA KUTOSHA; MNAANGAZA MAISHA YA WANANCHI” – MHE. KIKWETE


NA MWANDISHI WETU

Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwan Kikwete ameipongeza Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwa kuendelea kuhamasisha Matumizi ya Nishati Safi kwa Wananchi pamoja na kuimarika kwa upatikanaji wa huduma za nishati nchini.

Kikwete amesema hayo Juni 17, 2026  alipotembelea Banda la Wizara ya Nishati na Taasisi zake wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika Katika viwanja vya Chinangali jijini   Dodoma.

 Aidha, amesisitiza Wizara pamoja na Taasisi zake kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu Matumizi ya Nishati Safi ili Kila mmoja aifahamu kwa kina kwa manufaa  ya kulinda Afya na mazingira.

" Hongerani Sana Nishati kwa kuendelea kuwasha Umeme na kuangaza Maisha ya Wananchi, tunaona Umeme upo wa kutosha" Alisema Kikwete 

Sambamba na hilo amesisitiza  kuendelea kutangaza fursa zilizopo katika Sekta ya Nishati nchini kwa wananchi.

Ametembelea Taasisi  zilizo chini ya Wizara ya Nishati ambazo ni TANESCO, REA, TPDC, EWURA, PURA,PBPA na EWURA CCC ambapo alipata fursa ya kujionea huduma zinazotolewa na taasisi hizo pamoja na mafanikio ya miradi mbalimbali inayotekelezwa.


Post a Comment

0 Comments