*Watakiwa kutunza vyombo vya usafiri ili kuongeza ufanisi wa huduma
*TANESCO yanunua vyombo vya usafiri 982 kuimarisha utoaji wa huduma nchini
NA MWANDISHI WETU, LONGIDO
Madereva wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wamehimizwa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa kutunza vyombo vya usafiri vinavyotumika kuwafikia wateja kwa haraka na kwa ufanisi.
Rai hiyo imetolewa Julai 21, 2026 na Meneja wa Udhibiti wa Vihatarishi , Bw. Patrick Mbosa, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Madereva wa TANESCO 2026 Mkoani Iringa.
Amesema Shirika limewekeza katika ununuzi wa jumla ya vyombo vya usafiri 982, vikiwemo malori, magari madogo, bajaji na pikipiki, kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi katika maeneo yote nchini bila kujali changamoto za kijiografia.
"Hili ni jukwaa muhimu la kujikumbusha wajibu wetu. TANESCO imenunua vyombo vya usafiri 982 kwa ajili ya kuwahudumia wananchi. Ni wajibu wetu kuvitunza na kuzingatia sheria na usalama barabarani ili kuepuka ajali zisizo za lazima na kuhakikisha vinaendelea kutoa huduma kwa ufanisi na kwa muda mrefu," amesema Bw. Mbosa.
Kwa upande wao, baadhi ya madereva walioshiriki mkutano huo, akiwemo Bi. Gillian Ngowi na Bw. Joseph Mwanjalila, wamelishukuru Shirika kwa kuendelea kuboresha mazingira ya kazi na maslahi yao, jambo ambalo limeongeza ari ya kutekeleza majukumu kwa kujituma zaidi.
Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Madereva wa TANESCO 2026 ulianza Julai 20 na unatarajiwa kuhitimishwa Julai 24, 2026, ukiwa na kaulimbiu isemayo: "Madereva Wenye Maadili, Maendeleo kwa Shirika Letu."


.jpg)
0 Comments