GSM YAJITOA KUDHAMINI LIGI KUU YA NBC


NA ABRAHAM NTAMBARA
UONGOZI wa Kampuni ya GSM umetangaza rasmi kujiondoa kwenye nafasi ya kuwa mdhamini mwenza wa Ligi Kuu ya NBC yaani NBC Premier League.

Akizungumza na waandishi wa habari Afisa Biashara Mkuu wa GSM Allan Chonjo amesema sababu kubwa iliyofanya hata kufikia maamuzi hayo ni kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) pamoja na Bodi ya Ligi kushindwa kutekeleza baadhi ya vipengele vya kimkataba kama pande hizo mbili zilivyokubaliana.

“Ikumbukwe kuwa, GSM ilishawishika sana na TFF pamoja na Bodi ya Ligi na kuridhia kuwa mdhamini mwenza wa Ligi Kuu ili kukuza sekta hii ya mpira wa miguu hapa nchini pamoja na michezo kwa ujumla lakini hii halikuenda kama ilivyokusudiwa,” amesema Chonjo.

”Haya hayajawa maamuzi rahisi kwa kampuni ya GSM kwani tunatambua ya kuwa vipo baadhi ya vilabu vya mpira vitakavyoumizwa pamoja na wadau mbalimbali na hatua hii na wala haikuwa dhamira yetu kufikia uamuzi huu mgumu,” ameongeza Chonjo.

Hata hivyo Chonjo amesema GSM inapenda kuishukuru TFF, Bodi ya Ligi, Vilabu vyote pamoja na wadau wote kwa kuwa sehemu ya kuendeleza Sekta ya michezo hapa nchini.
Amesema “Tunapenda kuwatakia kila la kheri wadau wote wa mpira, mashabiki na wana michezo wote katika kuendeleza mchezo huu pendwa na tunawashukuru wote kwa kutuamini,”.

Amebainisha kwamba milango ya GSM bado ipo wazi kwa wadau wa michezo kuendelea kushirikiana nao katika kuendeleza tasnia hii na michezo mingine kwa manufaa ya Taifa la Tanzania.

Katika hatua nyingine Ghalib Said Mohamed ambaye ni Mwenyekiti na Mjumbe wa Kamati ya Ushindi ya tamu ya Taifa (Taifa Stars) amejiuzulu nafasi ya Mwenyekiti pamoja na mjumbe wa kamati hiyo.
@@@

Post a Comment

1 Comments