Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri wa Mazingira, Mhe. Reuben Kwagilwa, ametembelea mabanda mbalimbali ya taasisi na wadau wanaoshiriki Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani 2026 yanayofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre (JKCC), jijini Dodoma.
Katika ziara hiyo, Mhe. Kwagilwa amepata fursa ya kujionea shughuli, huduma na teknolojia mbalimbali zinazochangia uhifadhi wa mazingira, matumizi endelevu ya rasilimali za asili pamoja na juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Ametoa pongezi kwa taasisi na wadau wanaoshiriki maonesho hayo kwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira na kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira katika shughuli za kila siku.
Aidha, amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wananchi ni muhimu katika kufanikisha juhudi za uhifadhi wa mazingira na kufikia malengo ya maendeleo endelevu ya Taifa.
Akiwa katika banda la Wizara ya Nishati na taasisi zake za TANESCO, REA na TPDC, Mhe. Kwagilwa alipokea maelezo kuhusu mchango wa sekta ya nishati katika kuhifadhi mazingira kupitia matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na teknolojia ya Gesi Asilia iliyoshindiliwa kwenye Magari (CNG) ambapo alielezwa kuwa matumizi ya CNG yanaendelea kuhamasishwa nchini kama sehemu ya jitihada za kupunguza uchafuzi wa mazingira, sambamba na kuimarisha matumizi ya nishati safi na endelevu.
Aidha, alijionea teknolojia na huduma mbalimbali zinazotolewa na sekta ya nishati katika kuunga mkono agenda ya uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya kijani.
Mhe. Kwagilwa amewataka wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi za uhifadhi wa mazingira kwa kuzingatia kaulimbiu ya mwaka huu, “Dira 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania.”
Maonesho hayo yameanza rasmi leo tarehe 1 Juni 2026 na yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 5 Juni 2026, sambamba na maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani. Katika kipindi hicho, wananchi wanaendelea kutembelea mabanda ya Wizara ya Nishati ili kupata elimu kuhusu uhifadhi wa mazingira, matumizi ya nishati safi ya kupikia , teknolojia ya CNG na suluhisho nyingine rafiki kwa mazingira.




0 Comments